Baada
ya wiki kadhaa zilizopita kupata mtikisiko wa migomo ya wafanyakazi
wake, Shirika la ndege la Kenya limetangaza hasara ya shilingi bilioni
4.7 katika kipindi cha miezi sita kilichomalizika Septemba 30 mwaka huu.
Taarifa
iliyotolewa na shirika hilo la Serikali imesema pamoja na hasara hiyo
bado kuna unafuu ikilinganishwa na ile ya shilingi bilioni 11.9 ambayo
shirika hilo ilipata katika kipindi sawa na hicho mwaka 2016. Matokeo
hayo yanaonyesha kuwa kampuni hiyo imepunguza pengo la hasara kwa
asilimia 60.
Kupungua
kwa hasara hiyo kumechangiwa na ongezeko la abiria waliotumia ndege za
shirika hilo hadi kufikia abiria milioni 2.2 ikiwa ni ongezeko la
asilimia 4 ambapo ni sawa na abiria elfu 89 ikilinganishwa na kipindi
kama hicho mwaka jana.
Taarifa
hii imekuja wakati ambapo shirika hilo limekuwa likijaribu kila njia
katika kukabiliana na changamoto mbali mbali ili kuboresha mapato yake.
Katika
kipindi cha miezi sita iliyopita, shirika hilo lilipata mkopo wa
shilingi bilioni 9.8 kutoka kwa serikali ya Kenya ili kufanikisha juhudi
za kulikwamua kutoka kwa matatizo inayokabiliwa nayo.