Paparazi tzd

Hamisa Mobetto Afunguka Haya... Kuhusu Tetesi za Bifu Lake na Zari Hassan

Hamisa Mobetto amefunguka juu ya mahusiano yake na first lady wa Madale, Zari The Bosslady baada ya tetesi za kutoka na Diamond.

Mrembo huyo amemuambia mtangazaji wa kipindi cha The Playlist cha Times FM, Omary Tambwe aka Lil Ommy kuwa hajawahi kuwa na urafiki na Zari na wala hawana uadui wowote.

“Unajua huwezi kusema kuwa mimi na Zari tuko sawa au hatupo sawa kwa sababu hatujawahi kuwa marafiki, na mimi nimemjua kwa sababu ‘Kazaa’ na bosi wangu [Diamond Platnumz],” amesema Hamisa.

Malkia huyo wa video ya Salome ameongeza kuwa amewahi kuonana na Zari mara moja pekee ambapo ilikuwa ni kwenye 40 ya Tiffah mwaka jana.

JINA LA MAKONDA LATUMIKA KUTAPELI MAMILIONI.. SOMA HAPA

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es-Salaam limetoa tahadhari kwa wakazi wa kanda hiyo pamoja na wageni kutoka nje ya mkoa wa Dar es Salaam kwamba kuna baadhi ya matapeli wanatumia majina ya viongozi wa serikali kujipatia fedha kinyume na sheria za nchi.

Kamishna wa kanda hiyo, Kamanda Simon Sirro  wakati akizungumza na waandishi wa habari jana alisema kuwa jeshi hilo hivi karibuni limepokea malalamiko kutoka kwa raia wa kigeni kuwa kuna wahalifu wanalitumia jina la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda kuwataka watoe fedha kwa madai ya kuwasaidia wanafunzi kupata vyuo nje ya nchi.

Alieleza kuwa, mnamo Oktoba mosi mwaka huu raia wa china Marco Li mfanyakazi wa kampuni ya Group six International alipigiwa simu na mtu aliyejitambulisha kama Makonda na kumtaka atoe kiasi cha dola za kimarekani 3500.

Alisema tukio lingine lilitokea Oktoba 6, 2016 mkurugenzi wa kampuni hiyo Jensen Huang aliitumia fursa hiyo kumwomba mkuu wa mkoa huyo bandia kwamba amsaidie kumwidhinishia kuongezwa muda wake wa kuishi nchini ambao ulikuwa umeisha, na kwamba mhalifu huyo alimtaka atoe dola za kimarekani 7000 sawa na sh. Milioni 15.2.

Kamanda Sirro amewataka wakazi wote wa Dar es Salaam na wageni kuwa makini na matapeli hao na wakiona dalili za utapeli watoe taarifa katika vituo vya polisi kwa msaada zaidi ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheria.

Afungwa Jela Mwaka Mmoja kwa Kumdhalilisha Mama Yake Mzazi


Mwanaume mkazi wa Ilala, Siwema Seif (40) amehukumiwa na Mahakama ya Mwanzo ya Ilala kwenda jela mwaka mmoja kwa kumtolea lugha ya matusi na kumdhalilisha kimwili, Zainab Ramadhan ambaye ni mama yake mzazi.

Akisoma hukumu mahakamani hapo jana, Hakimu wa Mahakama hiyo, Matrona Luanda alisema ushahidi uliotolewa na shahidi namba moja ambaye ni mlalamikaji, ulionesha kukosa shaka na kumtia hatiani mshitakiwa.

Shahidi huyo alisema siku ya tukio mshitakiwa alifika nyumbani kwao akaomba chakula akajibiwa kuwa kuna wali na mshitakiwa akasema hataki wali bali anataka ugali na mama akamjibu asingeweza kupika ugali na kumsisitiza Siwema ale wali.

Zainab alisema baada ya majibizano hayo, mshitakiwa alimtukana matusi ya nguoni mama yake, huku akisema hawezi kumzaa na kumkashifu, kwamba hana sehemu ya kumzalia huku akitishia kumwua akiahidi kumtoa roho ndipo amjue yeye ni nani.

Kwa mujibu wa Zainab, alipoona ugomvi na matusi umezidi aliingia chumbani mwake, na ndipo mlalamikaji akamfuata na kumtukana huku akitishia kumwingilia kinyume cha maumbile.

“Baada ya hapo mshitakiwa alinivamia na kunidhalilisha kimaumbile kwa mikono yake,” alisema.

Baada ya ushahidi wa mama huyo dhidi ya Siwema, Mahakama ilitoa nafasi kwa kijana huyo kujitetea na Mahakama ikamtia hatiani.

Karani wa mahakama hiyo, Blanka Shao alisema kwa kuwa mshitakiwa alikuwa mkosaji wa mara ya kwanza na kitendo alichokifanya ni cha kifedhuli tena haonyeshi kujutia, alishauri apewe adhabu kali ili iwe fundisho kwake.

Hakimu Luanda alimhukumu kwenda jela mwaka mmoja kwa kitendo alichomfanya mama yake mzazi.

Awali, ilidaiwa mahakamani hapo, kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo Agosti 9 Ilala, mtaa wa Sophia Kawawa, nyumba namba 10.

Wahariri wamuangukia Rais Magufuli., Wamtaka Amshughulikie Serukamba Kwa Kuvuruga Muswada wa Habari


Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limemwomba Rais John Magufuli kumshughulikia Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Peter Serukamba kwa maelezo kuwa ni ‘jipu’ ambalo limevuruga mjadala wa Muswada wa Huduma za Habari.

Hayo yalibainishwa jana Dar es Salaam wakati wahariri wa vyombo vya habari walipokuwa wakijadili vipengele vya Muswada huo ambavyo vinatakiwa kufanyiwa mabadiliko kabla ya kupitishwa kuwa sheria kwa kuwa si rafiki kwa tasnia ya habari nchini.

Mhariri Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya New Habari Limited, Absalom Kibanda alisema Serukamba ni ‘jipu’ na kumwomba Rais aamini hivyo, akibainisha kwamba kipindi cha aliyekuwa Waziri wa Habari, Fenella Mukangara walipeleka hati ya dharura kutaka Muswada huo ujadiliwe vizuri, lakini alikataa huku akiunga mkono kama ulivyo.

“Kuna sauti ilisikika ikitembea katika mitandao, nikajiuliza ameongea kama Waziri, Ofisa Habari wa Serikali au mtu binafsi?” Alihoji Kibanda.

Kibanda alimwomba Rais aangalie ni nani wasemao ukweli kati ya wadau wa habari (wahariri na waandishiwa habari) na mamlaka nyingine za Serikali kuhusu namna nzuri ambayo Muswada huo unaweza kujadiliwa na kuwa sheria kwa maslahi ya Taifa bila kukwaza upande.

Aidha, alibainisha kuwa kuna watendaji wa Serikali ambao wamekuwa wakimsukuma Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo, ili aridhie mahitaji yao kwa maslahi binafsi.

Alisema kwa sasa waandishi wa habari wanafananishwa na wahalifu na kusema hivi karibuni walichapisha habari kwenye gazeti lao na walikuja kuomba radhi baada ya kupokea vitisho.

Aliongeza kuwa Muswada huo ulitakiwa uwekwe vipengele vinavyowachukulia hatua watu wanaoingilia kazi za vyombo vya habari, kwa kuwa makosa mengi vinayotupiwa vyombo vya habari vyanzo huwa ni wanasiasa.

Mjumbe wa TEF, Jesse Kwayu alisema wana wasiwasi na msimamo wa Serukamba, kwa kuwa anashindwa kutimiza majukumu yake ya kuisimamia Serikali na badala yake anakuwa kama ni ofisa wa Serikali.

“Wakati akiusoma Muswada huu kwenye Kamati, akihitimisha alisema hakuna uhuru usio na mipaka,” alisema Kwayu.

Alibainisha kuwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo aliyepita, alisikiliza vizuri mapendekezo ya wadau wa habari na kuyafikisha bungeni yajadiliwe tofauti na wa sasa ambaye si msikivu.

Alisema wakati wakiujadili hivi karibuni Dodoma ilifika mahali kukawa na mvutano mkali kati ya Serukamba na Zitto Kabwe kwa kuwa alikuwa hajaridhishwa na namna Muswada huo ulivyojadiliwa, kwa sababu wadau wa habari wahusika hawajahusishwa kikamilifu.

Alisema asilimia 80 ya waandishi wa habari wako mikoani ambako waandishi hao pia hawajajadili na kupata mwafaka wa Muswada huo.

Naibu Mhariri Mtendaji wa Jamhuri, Manyerere Jackton aliwataka Serukamba na Mkurugenzi wa Idara ya Habari, MAELEZO, Hassan Abbas wasijisahau na kupitisha Muswada huo eti kwa kuwa wako serikalini, bali wajue kuwa kuna wakati watarudi na kukabiliwa na sheria hiyo.

Mwenyekiti wa TEF, Theophil Makunga alisema Muswada huo usipobadilishwa vipengele hivyo na ukapitishwa kuwa sheria, waandishi wa habari watakuwa kwenye shida kubwa kwa kuwa watakuwa wakipambana na kitu kibaya sana.

Wema Sepetu Amuandikia Ujumbe Huu Miss Tanzania Mpya

Miss Tanzania 2006, Wema Sepetu amedai mshindi wa shindano la Miss Tanzania 2016, Diana Edward alistahili kuchukua taji hilo.

Kupitia Instagram, Wema ameandika:

When You Nailed that question Properly, I knew that The Crown was Yours…. Congratulations mdogo wangu… You deserve it… And I have a very good feeling about Your performance in the Miss World Beauty Pageant…. You will do Tanzania Proud… @dianaflave @dianaflave @dianaflave @dianaflave … #GoodMorningWorld

Faraja Nyalandu aliyewahi kushika taji hilo naye amekuwa miongoni mwa watu waliompongeza mshindi huyo

RAIS MUSEVEN AKITOKA SHAMBANI KULIMA, JIONEE MWENYEWE HAPA

Rais wa Uganda Yoweri Museveni amerudi shambani kwake ambapo atakuwa kwa kipindi cha juma moja akikuza kilimo mbali na kusimamia miradi ya serikali katika wilaya ya Lowero.Rais wa Uganda na msafara wake akielekea shambani
Msafara wa rais sasa utakuwa wa baiskeli kwa muda ambayo atatumia kuteka maji ili kunyunyizia mimea.
Rais wa UgandaKulingana na msemaji wa serikali,Museveni tayari amekuwa akiwaonyesha wakaazi jinsi ya kupanda migomba na kahawa kwa kutumia chupa za plastiki ili kunyunyizia maji.

TAARIFA KUHUSU WACHINA WALIOMTEKA NA KUMPA KICHAPO MCHINA MWENZAO

Raia watatu wa China wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashitaka ya kumteka na kumjeruhi raia mwenzao, Liu Hong.

Washitakiwa hao, Chen Chuw Bao (34), Wang Yong Jim (37) na Zheng Pa Jin (40) wamefikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidi, Cyprian Mkeha.

Wakili wa Serikali, Hellen Moshi alidai kuwa Oktoba 21, mwaka huu katika maeneo ya Palm Beach Ilala, Dar es Salaam Wachina hao walimteka raia mwenzao wa China, Liu Hong ili kumuweka kizuizini.

Alidai kuwa siku hiyo katika maeneo hayo ya Palm Beach, washitakiwa walimshambulia Hong katika sehemu za mwili na kusababisha apate maumivu ya misuli.

Baada ya kusomewa mashitaka Bao alikiri kutenda makosa yote, huku Jim akikiri kosa moja na Jin alikana mashitaka yote.

Wakili Moshi alidai kuwa amepokea taarifa kutoka kwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Kipolisi Ilala, Dar es Salaam, SSP Salum Ndalama akiiomba Mahakama isitoe dhamana kwa washitakiwa hao.

Wakili Moshi alidai SSP Ndalama ametoa zuio hilo kwa kuwa washitakiwa hao ni raia wa China, pia hawana kazi wala hati za makazi ya kudumu.

Aidha, kuna taarifa za kuaminika kwamba washitakiwa hao na watuhumiwa wengine ambao hawajakamatwa wanapanga njama za kujihusisha na vitendo vya kihalifu ukiwemo utekaji.

Alidai washitakiwa hao na wengine ambao hawajakamatwa wana mpango wa kulipiza kisasi na endapo wakipata nafasi ya kupewa dhamana, wanaweza kwenda kupoteza ushahidi.

Wakili huyo, aliongeza kuwa rai ya SSP Ndalama ni kuwa, washtakiwa hao waendelee kubaki rumande hadi kesi hiyo itakapoisha ili kumlinda majeruhi pamoja na ushahidi. Baada ya kueleza hayo, Hakimu Mkeha aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 11, mwaka huu

MITIHANI YA KIDATO CHA NNE IMEANZA LEO, HII NDIO IDADI YA WATAHINIWA

Watahiniwa 408,442 wamesajiliwa na Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) kufanya Mtihani wa Kidato cha Nne unaotarajia kuanza leo hadi Novemba 18, mwaka huu.

Akizungumzia maandalizi ya mtihani huo, Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde alisema kati ya watahiniwa waliosajiliwa wa shule ni 355,995 na wa kujitegemea ni 52,447. Mwaka 2015, waliosajiliwa kufanya mtihani ni 448,382, hivyo kuwapo na upungufu wa watahiniwa 39,940.

Dk Msonde alisema kati ya watahiniwa wa shule 355,447 waliosajiliwa, wavulana ni 173,423 ambao ni asilimia 48.72 na wasichana ni 182,572 sawa na asilimia 51.28. Watahiniwa 59 ni wasioona na wenye uoni hafifu ni 283.

Alisema kati ya watahiniwa wa kujitegemea 52,447 waliosajiliwa, wanaume ni 25,529 sawa na asilimia 48.68 na wanawake ni 26,918 sawa na asilimia 51.32.

Pia watahiniwa wa kujitegemea wasioona wako saba, wanawake watatu na wanaume ni wanne. Mwaka jana watahiniwa wa kujitegemea walikuwa ni 54,317.

Kuhusu watahiniwa waliosajiliwa kufanya Mtihani wa Maarifa (QT), Dk Msonde alisema baraza limesajili 20,634 ambao wanaume ni 7,819 sawa na asilimia 37.89 na wanawake ni 12,815 sawa na asilimia 62.11. Mwaka jana, idadi ya watahiniwa wa QT walikuwa 19,547.

“Maandalizi yote kwa ajili ya mtihani huo yamekamilika ikiwa ni pamoja na usambazaji wa mtihani, vitabu vya kujibia na nyaraka zote muhimu zinazohusu mtihani huo katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani,” alieleza Dk Msonde.

Aidha, baraza limewaasa wanafunzi, walimu kutojihusisha na vitendo vya udanganyifu wa mtihani kwani watakaobainika kufanya hivyo watachukuliwa hatua kali zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kufutiwa matokeo yote.

Katika matokeo ya darasa la saba yaliyotangazwa wiki iliyopita, wanafunzi 238 kutoka shule sita walifutiwa matokeo yao yote kutokana na udanganyifu wa mtihani.

Dk Msonde alizitaka Kamati za Mitihani za Mikoa na Halmashauri, kuhakikisha kuwa taratibu zote za uendeshaji mitihani ya Taifa zinazingatiwa ipasavyo, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa mazingira ya vituo yapo salama, tulivu na kuzuia mianya yote inayoweza kusababisha udanganyifu. Pia Dk Msonde alitoa mwito kwa wasimamizi wote kufanya kazi yao kwa umakini na uadilifu wa hali ya juu.

“Wasimamizi wanaaswa kujiepusha na vitendo vya udanganyifu kwani baraza litachukua hatua kali kwa yeyote yule atakayebainika kukiuka taratibu za uendeshaji wa Mitihani ya Taifa,” alieleza.

MAGAZETI YA LEO JUMANNE NOVEMBER 1, 2016.. YASOME HAPA


Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumanne ya Novemba 1

Barabara yapewa jina la Kikwete Nairobi

Barabara ya Jakaya Kikwete
Serikali ya kaunti ya Nairobi nchini Kenya imebadilisha jina la barabara moja na kuipa jina la Rais wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete.
Kiongozi huyo alikuwa nchini Kenya kwa ziara ya siku tatu na Jumanne alihutubia kikao cha pamoja cha Bunge la Seneti na Bunge la Kitaifa.
Rais Kikwete alihudhuria sherehe ya kubadilisha jina barabara hiyo ya Milimani iliyoko karibu na ikulu ya Nairobi.
Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 0.49 huanzia makutano ya barabara ya Kenyatta Avenue na Valley Road na kufululiza hadi barabara ya Dennis Pritt.
"Rais Kenyatta aliposema kwamba utazuru hapa tulishauriana kujua iwapo tungeweza kubadilisha jina la barabara hii na kwa kuwa sisi ni marafiki, alikubali, na kama uonavyo, inaelekea hadi lango la ikulu yake (Bw Kenyatta),” Gavana wa Nairobi Dkt Evans Kidero alimwambia Bw Kikwete, kwa mujibu wa gazeti la The Star la Kenya.
Barabara hiyo imo karibu na barabara ya Nyerere.
Rais Kikwete sasa anajiunga na kiongozi wa kwanza wa Tanzania Julius Nyerere na Rais wa kwanza wa Zanzibar Sheikh Abeid Karume katika kuwa na barabara zilizopewa majina yao Nairobi.
Kabla ya kuondoka mamlakani mwaka 2013, aliyekuwa rais wa Kenya wakati huo Mwai Kibaki, alibahatika kuwa na barabara yenye jina lake jijini Dar es Salaam.
Sherehe ya kubadilisha jina la barabara hiyo ya Old Bagamoyo ilihudhuriwa na Bw Kibaki mwenyewe, Rais Kikwete na Bw John Magufuli aliyekuwa waziri.
Bw Magufuli kwa sasa ni mgombea wa urais wa chama tawala cha CCM.

Mwanamke mwenye 'macho ya kushangaza' akamatwa

Steve McCurry na picha za Sharbat Gula Hamburg, Ujerumani Juni 27, 2013.
Mhamiaji kutoka Afghanistan, ambaye alipata umaarufu picha yake ilipochapishwa kwenye ukurasa wa kwanza wa jarida la National Geographic miaka thelathini iliyopita, amekamatwa.
Maafisa wanasema amekamatwa kwa kuwa na nyaraka bandia za utambulisho.
Sharbat Gula alipata umaarufu mwaka 1985 kutokana na picha hiy aliyopigwa akiwa na umri wa miaka 12.
Macho yake yalikuwa na rangi ya kijani, jambo lililomfanya kufahamika kwa jina 'Green-eyed Girl'.
Maafisa wanasema alikamatwa na Idara ya Uchunguzi ya Pakistan (FIA) baada ya uchunguzi wa miaka miwili Peshawar, karibu na mpaka wa nchi hiyo na Afghanistan.
Pakistan ilianza kuwasaka watu wenye vitambulisho bandia majuzi.
Bi Gula aliwasilisha ombi la kutaka kitambulisho Aprili 2014 akitumia jina Sharbat Bibi.
Iwapo madai hayo yatathibitishwa, basi atakuwa mmoja wa maelfu ya wakimbizi kutoka Afghanistan ambao wamejaribu kukwepa mfumo wa usajili wa watu unaotumia kompyuta nchini Pakistan.
Afisa wa Mamlaka ya Taifa ya Usajili wa Watu (Nadra) amesema maafisa wa FIA pia wanawatafuta wafanyakazi watatu ambao wanadaiwa kumpa kitambulisho Bi Gula.
Gazeti la Dawn la Pakistan limesema Bi Gula alipewa vitambulisho pamoja na wanaume wengine wawili waliodai kuwa wanawe wa kime.

PICHA 3: Rais Magufuli alivyowasili Nairobi nchini Kenya

Leo October 31 2016 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli aliondoka nchini kuelekea Nairobi nchini Kenya kwa ziara ya Kiserikali ya siku mbili nchini humo kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Kenya Uhuru Kenyatta.
Rais  Magufuli  amewasili Nairobi kenya kwa ziara hiyo na amelakiwa na mwenyeji wake Rais uhuru kenyatta.
tza-ke-rais-magufuli-nchini-ke
tza-ke-rais-magufuli-nchini-ke-3jpg

Lukuvi Afafanua Jinsi Utapeli wa Ardhi Unavyofanyika

Waziri wa ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi, William Lukuvi, ameeleza jinsi matapeli wa ardhi wanavyoshirikiana na baadhi ya maafisa ardhi hasa wa halmashauri za manispaa na jiji kutekeleza utapeli wa ardhi kwa kutumia barua bandia.

Lukuvi ameeleza hayo wakati akihojiwa katika kipindi cha ‘KUMEKUCHA’ kinachorushwa na kituo cha runinga cha ITV.

“Mtu akinunua ardhi hupewa karatasi za ofa ambazo hivi sasa zilizojaa ni feki, lakini wapo wajanja na matapeli wanatumia ofa hizo kudhulumu viwanja vilivyo wazi. Mfano wakiona kiwanja kipo wazi wanakwenda katika halmashauri wanashirikiana na baadhi ya maafisa ardhi wasio waaminifu, wanauliza namba ya ploti ya kiwanja husika na anayemiliki,” alisema.

“Wakishajua namba na mmiliki wa kiwanja huiondoa ofa halali katika faili kisha afisa ardhi anaiweka feki, siku mmiliki halali akienda kuulizia kiwanja chake katika halmashauri anakuta ofa yake haipo ipo ya mtu mwingine ambaye ameghushi tarehe ya barua ya ofa,”aliongeza.

Aidha Lukuvi alisema matapeli wa ardhi huyafahamu maeneo yaliyo wazi na kwamba asilimia kubwa hushughulika na yale ambayo wamiliki wake wamefariki dunia.

“Hawa matapeli huyajua maeneo vizuri, na wanachokifanya ni kutengeneza ofa feki kisha kuziweka katika faili za halmashauri, ukienda mmiliki halali unaambiwa ni tapeli kwa kuwa barua yako haiko katika faili,” amesema na kuongeza,”Matapeli wanaishi mjini kwa kutengeneza ofa bandia, wastaafu,yatima na wajane wanalizwa kila siku,” amesema.

Ametoa agizo kwa maafisa ardhi wa kanda kutotoa huduma wala kushugulika na barua za ofa kwa sababu baadhi yao ndio wanaobadilisha ofa halali za watu.

Faraja Kotta Azungumza Hili Baada ya Miss Tanzania 2016 Diana Edward Kuandamwa Mitandaoni

Aliyewahi kuwa mshindi wa Miss Tanzania kwa mwaka 2004, Faraja Kotta Nyalandu amechukizwa na yale yanayoendelea katika mitandao ya kijamii juu mshindi wa taji la Miss Tanzania 2016, Diana Edward.
faraja

Hatua hiyo imekuja baada ya watu katika mitandao ya kijamii kuanza kumshambulia mshindi huyo juu ya umri wake. Hata hivyo kamati ya Miss Tanzania ilitolea ufafanuzi juu ya suala hilo.

Miss Faraja Kotta ambaye na yeye pia alipitia kipindi kigumu pindi alipotangazwa mshindi, ameandika ujumbe huu:


"Niliposhinda Miss Tanzania, kuna mtangazaji fulani (tena wa kiume) wa kipindi cha redio cha asubuhi alitumia kama saa nzima hewani kusema ambavyo sikustahili kushinda. Asubuhi ya Jumatatu kama leo baada ya weekend ya shindano.

Nilipigiwa simu kuamshwa. Nakumbuka niliamka nikawasha redio na nikasikiliza kipindi chote, peke yangu, chumbani.
Nilitetemeka, nilishindwa kuoga, kula, nilijifungia ndani siku nzima nikilia. Niliwaza sana ambavyo pengine ni kweli sikustahili. Nilijuta kushiriki Miss Tanzania.

I was young and naive. I had just turned 19, coming straight from the safety nets of Catholic nuns boarding schools. Sikujua kuna watu wanaweza kuwa na roho mbaya hata kwa watu wasiowajua.

It took my parents (RIP) na kila busara waliyonayo kunifanya nijisikie vizuri. I had to dig deep inside me to regain my purpose. I was exposed to a cruel world and yes, I quickly learnt, it is what it is.

Leo hii hakuna binadamu mwenye hiyo nguvu niliyompa yule mtangazaji. I learnt the hard way but I am grateful for the lesson. Thank God I learnt early. Kuna sehemu ya nguvu niliyo nayo leo iliyotokana na kujeruhiwa na binadamu na kupona. Lakini si kila mtu atapata bahati ya kupona, unaweza kumjeruhi mtu na akapotea moja kwa moja. Usijitafutie laana za reja reja.
To the newly crowned Miss Tanzania, Do you honey!

To the rest of us, tujenge zaidi ya kubomoa. Love doesn’t cost a thing!
God bless,
Faraja"

Picha: : Rais Magufuli aondoka Nchini Kwenda Kenya Kwa Ziara ya Kiserikali ya Siku Mbili

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 31 Oktoba, 2016 ameondoka nchini kuelekea Nairobi nchini Kenya kwa ziara ya Kiserikali ya siku mbili nchini humo kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Uhuru Kenyatta.

Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, Rais Magufuli ameagwa na viongozi mbalimbali wa serikali akiwemo Makamu wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi, Mkuu wa Mkoa wa Dar Es salaam, Paul Makonda na viongozi mbalimbali wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama.

Mara baada ya kuwasili nchini Kenya, Rais Magufuli atafanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta, na baadae atakwenda kutoa heshima katika Kaburi la Rais wa Kwanza wa Kenya Hayati Mzee Jomo Kenyatta.

Mheshimiwa Rais pia anatarajiwa kuhudhuria dhifa ya kitaifa atakayoandaliwa na mwenyeji wake Ikulu Jijini  Nairobi.

Katika ziara hiyo Rais Magufuli anatarajiwa kutembelea kiwanda cha maziwa cha  Eldoville kilichopo Karen Jijini Nairobi na pia kuzindua barabara mchepuko (Southern By-pass) iliyopo Jijini humo. Barabara hiyo ni moja kati ya miradi mikubwa ya barabara nchini Kenya, inayounganisha maeneo mbalimbali ya Jiji la Nairobi kwa barabara za juu na chini.

Jaffar Haniu
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar Es Salaam

31Oktoba, 2016
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akisindikizwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere akiwa tayari kwa safari ya kwenda Nairobi, Kenya kwa ziara ya kiserikali ya siku mbili leo Oktoba 31, 2016. Hii ni safari yake rasmi ya tatu kwenda nje ya nchi toka aingie madarakani mwaka mmoja uliopita. Alisafiri kwa mara ya kwanza alikwenda Rwanda, kisha akaenda Uganda.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akisalimiana na Naibu Balozi wa  Kenya nchini Mhe Boniface Muhia katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere akiwa tayari kwa safari ya kwenda Nairobi, Kenya kwa ziara ya kiserikali ya siku mbili  leo Oktoba 31, 2016
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akipokea saluti toka kwa Inspekta jenerali wa Polisi (IGP) Ernest Mangu  katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere akiwa tayari kwa safari ya kwenda Nairobi, Kenya kwa ziara ya kiserikali ya siku mbili leo Oktoba 31, 2016
Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi,  Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda na viongozi wengine wakipunga mikono kumuaga Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli  katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere wakati akianza  safari ya kwenda Nairobi, Kenya kwa ziara ya kiserikali ya siku mbili leo Oktoba 31, 2016. PICHA NA IKULU

Lowassa, Sumaye Wapiga Kambi Dodoma Ili Kuteta na Wabunge wa UKAWA


Mawaziri Wakuu wa zamani ambao ni wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa na Frederick Sumaye wameweka kambi mjini Dodoma ili kuteta na wabunge wa Ukawa.

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano, Uenezi na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alisema kuwa wanasiasa hao wako mjini humo kwa ajili ya kufanya vikao na wabunge wa Ukawa ili kuweka mkakati na msimamo dhidi ya hoja mbalimbali zinazotarajiwa kuibuliwa katika vikao vya Bunge vinavyoanza kesho.

Moja kati ya hoja zinazotarajiwa kuwekewa msimamo ni pamoja na kuupinga muswada wa huduma za habari unaotarajiwa kujadiliwa na kupitishwa kuwa sheria.

“Tutakuwa na kikao cha kuweka msimamo wetu dhidi ya muswada hatari wa huduma za habari,” Mrema anakaririwa. “Vikao vimeshaanza na vitaendelea kesho (leo),”aliongeza.

Kwa mujibu wa Mrema, mbali na Lowassa, Sumaye na mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, vigogo wengine wa Ukawa waliohudhuria vikao hivyo ni pamoja na Profesa Mwesiga Baregu, Profesa Abdallah Safari na Arcado Ntagazwa.

SERIKALI YAWAZUIA MCHUNGAJI LWAKATARE NA MREMA KUWALIPIA FAINI WAFUNGWA

Serikali imesitisha shughuli iliyokuwa ikiendeshwa na Mchungaji Getrude Lwakatare ya kuwalipia faini wafungwa walioko magerezani hadi hapo utaratibu mwingine utakapotolewa.
Mpango huo unaofanywa na Lwakatare kwa kushirikiana na Mwenyekiti wa Taifa wa Bodi ya Parole, Augustine Mrema tayari umewezesha wafungwa 78 kutoka magerezani baada ya kuwalipia faini inayofikia Sh25 milioni. 
Mkuu wa Magereza Mkoa wa Dodoma, Antonio Kilumbi alisema amepata maelekezo ya kusitishwa kwa mpango huo kutoka ngazi ya juu ya jeshi hilo. 
Alisema wananchi wengine bado wanaweza kuwalipia faini hiyo ndugu zao. Mrema alisema jana kuwa mpango huo ulilenga kupunguza msongamano magerezani na kuipunguzia Serikali gharama za kuwahudumia wafungwa.

TAARIFA YA SERIKALI KUHUSU TUHUMA ZA KUUZA KISIWA CHA SHUNGI MBILI

Serikali  imewahakikishia wakazi wa Wilaya ya Mafia na Watanzania wote kuwa Kisiwa cha Shungi Mbili kilichopo wilayani humo mkoani Pwani, hakijakodishwa wala kuuzwa kwa mtu yeyote kama inavyodaiwa na baadhi.

Badala yake, serikali imeingia mkataba na mwekezaji kwa ajili ya kufanya biashara ya hoteli ya kitalii ya hadhi ya nyota tano katika kisiwa hicho kwa kipindi cha miaka 20, uwekezaji ambao una manufaa zaidi kwa wananchi na serikali kwa ujumla.

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa hoteli hiyo iliyopewa jina la Thanda, Meneja Mkuu wa Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu nchini, Dk Milali Machumu alisema mwekezaji huyo ameingia mkataba huo na serikali kufanya biashara hiyo ikiwa ni sehemu ya kukiendeleza Kisiwa cha Shungi Mbili ambacho kilikuwa hakikaliwi na watu.

“Mimi niwahakikishie tu Watanzania kwamba serikali iliyoko madarakani chini ya Rais John Pombe Magufuli ipo makini na hizo tetesi za kuuzwa kwa kisiwa hiki mzipuuze, kwani kama mnavyoona pamejengwa hoteli ya kitalii kwa makubaliano na serikali na sio kuuzwa wala kukodishwa,” alisema Dk Machumu.

Alisema kufunguliwa kwa hoteli hiyo kutainufaisha serikali kwa kupata mapato kupitia kodi na kutengeneza ajira kwa wakazi wa Mafia pamoja na kuchochea maendeleo na pia wamezingatia sheria ya utunzani wa mazingira ya baharini.

Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Shaibu Nunduma alisema kufunguliwa kwa hoteli hiyo kumetoa fursa nzuri ya ajira kwa wakazi wake na pia kutachochea kasi ya maendeleo kwa wilaya hiyo.

Mkurugenzi Mkuu wa hoteli hiyo, Pierre Delvaux aliishukuru serikali kupitia kwa Meneja wa Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu, Dk Machumu kwa kuwezesha uwekezaji huo, ambao machakato wake ulianza miaka 10 iliyopita.

Delvaux alisema hoteli hiyo ina vyumba vitano vya kulala, bwawa la kuogelea, maeneo ya michezo kama tenisi pamoja na vitu vyote vya kufurahisha na gharama yake ni Dola za Marekani 10,000 (sawa na zaidi ya milioni 20) kwa usiku mmoja.

Pia alisema wamezingatia manufaa kwa wakazi wa Mafia na hivyo kwa upande wa ajira asilimia 65 itakuwa ni kwa wakazi wa kisiwa hicho.

“Leo tumeizindua rasmi hoteli hii, lakini itaanza kufanya kazi katikati ya Novemba mwaka huu,” alisema Delvaux.

Kisiwa cha Shungi Mbili ambacho ni sehemu ya Wilaya ya Mafia mkoani Pwani ni miongoni mwa visiwa 15 ambavyo ni maeneo tegefu vilivyopo katika Bahari ya Hindi na hairuhusiwa kufanya shughuli yoyote ya uvuaji wa samaki.

VIDEO, POLISI WANAVYOMPIGIA SALUTI LIPUMBA... ANGALIA HAPA

Kitendo cha askari polisi kumpigia saluti Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF) anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa, Profesa Ibrahim Lipumba imezua gumzo la kuhoji uhalali wake.

Askari huyo alionekana juzi akimpigia saluti Profesa Lipumba katika eneo la Buguruni ambapo mwanasiasa huyo alienda kushiriki zoezi la usafi.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Ilala, Salum Hamduni alipoulizwa kuhusu usahihi wa askari polisi kuwapigia saluti viongozi wa vyama vya siasa wasio wabunge alijibu kwa ufupi, “sio sawa.”

Kwa mujibu wa Kanuni za Jeshi la Polisi (PGO) namba 102, haiwataji viongozi wa vyama vya siasa wasio wabunge kati ya watu wanaopaswa kupewa salamu hiyo ya jeshi yenye kuonesha heshima.

Aliyekuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Kapteni John Chiligati aliwahi kueleza Bungeni kuwa saluti ni ishara ya kuonesha heshima kwa kiongozi mkuu kwenye asasi za kijeshi.

Kapteni Chiligati alisema kuwa mbali na viongozi wa kijeshi, viongozi wengine wanaopaswa kupewa saluti ni wa mihimili ya Serikali, Bunge na Mahakama.

Wengine ni majaji wote, wabunge, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na mahakimu wa mikoa na wilaya wakiwa kwenye mahakama zao.

Katibu Mkuu wa Chama Cha CCK, Renatus Muabhi alisema kuwa huenda askari huyo alipiga saluti kwa kupaniki kutokana na maagizo aliyopewa ya kumlinda Profesa Lipumba katika zoezi hilo.

TAARIFA MPYA KWA WANAFUNZI WA VYUO VIKUU WALIOKOSA MIKOPO

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetoa ufafanuzi kuhusu vigezo inavyotumia katika kuchambua, kupanga na kutoa mikopo kwa wanafunzi 20,183 (asilimia 74) wa mwaka wa kwanza hadi sasa kati ya 25,717 iliyopanga kuwapa mikopo katika mwaka huu wa masomo, 2016/2017.

Idadi iliyobaki (asilimia 26) ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza itajazwa na waombaji ambao baadhi ya nyaraka walizowasilisha zinaendelea kuchambuliwa ili kuthibitisha uhalisi wake na baadhi zitajazwa na waombaji ambao wanakata rufaa na kuwasilisha nyaraka zinazothibitisha uhitaji wao kwa mujibu wa vigezo vya mwaka huu.

Aidha, katika mwaka huu wa masomo, Serikali imepanga kutumia jumla ya Tshs 483 kutoa mikopo kwa wanafunzi 93,295 wanaoendelea na 25,717 wa mwaka wa kwanza.

Katika mkutano na waandishi wa habari jana (Jumapili, Oktoba 30, 2016), Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Bw. Abdul-Razaq Badru alisema vigezo vikuu vinavyotumika mwongozo uliotangazwa na Bodi hiyo wakati ilipotangaza kuanza kupokea maombi mwezi Juni mwaka huu ambao unataja makundi makuu matatu ya watakaopata mikopo.

Vigezo vilivyotumika kutoa mikopo
Kwa mujibu wa Bw. Badru, kundi la kwanza linajumuisha wanafunzi waombaji wa mikopo wenye uhitaji maalum kama wenye ulemavu uliothibitishwa na Waganga Wakuu wa Wilaya na yatima ambao katika maombi yao waliwasilisha nakala za vyeti vya vifo zilizothibitishwa na makamishna wa viapo.

“Kundi la pili linajumuisha waombaji wa mikopo ambao baada ya uchambuzi wa taarifa zao walizowasilisha na baada ya kulinganisha na gharama za jumla za masomo yao ya sekondari, wamebainika kuwa wana uwezo mdogo wa kugharamia masomo yao ya elimu ya juu na hivyo kuwa na uhitaji zaidi wa mikopo,”
alisema Bw. Badru.

Katika mkutano huo uliofanyika katika Ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Bw. Badru alitaja kundi la tatu na la mwisho kuwa linajumuisha waombaji wa mikopo ambao wenye ufaulu wa juu katika matokeo yao ya kidato cha sita na wamechaguliwa kujiunga na fani za kipaumbele kwa taifa.

Fani hizo ni Sayansi za Tiba, Ualimu wa Sayansi na Hisabati, uhandisi wa Kilimo, Mafuta na Gesi na Sayansi za Ardhi, Usanifu Majengo na Miundombinu.

Makundi ya wanafunzi waliopata mikopo
“Hivyo basi, hadi sasa tumetoa mikopo kwa wanafunzi 20,183 wakiwemo wanafunzi yatima 4,321, wenye ulemavu 118, wanafunzi wenye uhitaji waliosomeshwa na taasisi mbalimbali katika masomo ya sekondari (87), wanafunzi wanaosoma kozi za kipaumbele 6,159 na wanafunzi wanaosoma kozi zisizo za kipaumbele lakini wanaotoka kwenye familia duni 9,498,” alifafanua Bw. Badru. 

Sababu za kukosa mikopo
Katika mkutano huo, kiongozi huyo wa HESLB pia alieleza kwa kina sababu nyingine za waombaji 27,053 ambao hawajapangiwa mikopo.

Ametaja sababu hizo kuwa ni pamoja na baadhi ya waombaji (90) kuwa na umri wa zaidi ya miaka 30, waombaji mikopo waliopata udahili kwa sifa linganishi (equivalent qualifications) na waombaji waliomaliza masomo ya kidato cha sita zaidi ya miaka mitatu iliyopita.

Kundi jingine la waombaji waliokosa mikopo katika awamu ya kwanza ni waombaji waliopata nafasi katika vyuo kwa ufaulu wa mitihani waliyofanya kama watahiniwa binafsi (Private Candidates) na waombaji ambao hawakurekebisha fomu zao za maombi ingawa waliitwa kufanya hivyo.

Nafasi ya rufaa na uhakiki wa wanafunzi wanaoendelea na masomo
Katika mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji huyo pia amewataka waombaji ambao hawajaridhika na upangaji wa mikopo unaotangazwa, kuwasilisha rufaa zao kwa njia ya mtandao utakaofunguliwa kuanzia katikati ya wiki hii.

“Tunafahamu kuwa kuna baadhi ya wanafunzi wamekosa mkopo kwa kutowasilisha baadhi ya nyaraka ingawa tuliwaomba kufanya hivyo, hawa na wengine wenye sababu za msingi, watapata fursa ya kuwasilisha rufaa zao kwa njia ya mtandao na nakala kuzituma kwa utaratibu tutakaoutangaza wiki inayoanza kesho(leo),”
alisema Bw. Badru.

Aidha, katika mkutano huo, Bw. Badru alisema bodi ya Mikopo inatarajia kuanza kazi kuhakiki taarifa za wanafunzi wanaoendelea na masomo ambao wanapata mikopo ya elimu ya juu kwa lengo la kubaini kama ni wana uhitaji wa mikopo hiyo kwa mujibu wa vigezo au hapana.

Katika zoezi hili linalotarajiwa kufanyika kwa siku 30 kuanzia mwezi ujao (Novemba, 2016), wanafunzi wote ambao ni wanufaika watalazimika kujaza dodoso maalum litakalokusanya tarifa za kiuchumi za wazazi na walezi wao ili kuweza kupata uhalisia wa sasa.

“Wanafunzi watakutana na dodoso katika akaunti zao katika mtandao wetu wa maombi ya mikopo (OLAMS) na watapaswa kujaza. Wale ambao hawatajaza dodoso hili kwa njia ya mtandao tutasitisha mikopo yao na wale ambao baada ya uchambuzi tutabaini hawana uhitaji, nao tutasitisha mikopo yao na watapaswa kuanza kurejesha fedha walizokopokea,’ alifafanua.

HESLB ilianzishwa mwaka 2004 na kuanza kazi rasmi mwezi Julai mwaka 2005 kwa lengo la kutoa mikopo kwa watanzania wahitaji waliopata nafasi za masomo katika vyuo vya elimu ya juu na kukusanya mikopo iliyoiva kutoka kwa wadaiwa walionufaika na mikopo tangu mwaka 1994.